News

Horoya hatoki, kila dakika Simba Sh2 milioni

SIMBA imepania kurejea robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ili kuvuta mabilioni ya pesa kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na kuhakikisha hilo linatimia vigogo wa Msimbazi wametangaza bonasi mpya kwa wachezaji katika mchezo ujao dhidi ya Horoya ya Guinea ambao kama watashinda basi watakuwa wametoboa.

Tajiri kaweka milioni 200 mezani ambazo kwa hesabu ya kawaida ndani ya dakika 90 kwenye kila dakika watakayokuwa uwanjani watalipwa Milioni 2.2. Hapo bado ule mkwanja wa Rais Samia Suluhu haujaingia.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa Wachezaji wa kikosi hicho watawekwa kikao leo na kesho kuweka mikakati mizito pamoja na kutajiwa dau hilo ambalo mabosi akiwemo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya timu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ ambaye amewaeleza kuwa rais wa heshima na mfadhili wa timu hiyo Mohamed Dewji ‘Mo’ wamekubaliana. Wameongeza bonasi hilo kwenye mechi ijayo dhidi ya Horoya ambapo badala ya Mil 100 walizozowea sasa ni Mil 200 kama watashinda.

Mkwanja huo ni hamasa kuhakikisha Simba inafuzu robofainali wikiendi ijayo kwenye ardhi ya nyumbani badala ya kujiongezea ugumu kutegemea hesabu za vidole mechi za mwisho ugenini.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti imeambiwa ni kwamba, Simba ambayo ilishaenda robo mara mbili, wachezaji na benchi la ufundi walikuwa wakivuta bonasi ya hadi sh 150 milioni kama wakishinda mechi za ugenini na sh 100 milioni ikitoa sare ugenini huku ushindi kwenye mechi za nyumbani wakivuta 100 milioni na sare kuchukua 50 milioni bonasi ambayo katika mechi na Horoya imepanda na sasa watakuwa wakichukua milioni 200 kama watashinda.

Simba hawataki kutegemea matokeo ya mechi zingine, wamepania kuhakikisha wanamaliza kila kitu wenyewe na hapo akaunti za timu hiyo zitapokea zaidi ya bilioni moja kutoka CAF ikiwa ni bonasi ya kufika robo.

CAF hutoa bonasi kwa timu shiriki kuanzia hatua ya makundi ambapo kwa msimu huu timu zote zitazofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitapewa kitita cha dola 650,000 ambazo ni zaidi ya Sh 1.4 bilioni za Kitanzania.
Hivyo mabosi wa Simba hawataki kuukosa mkwanja huo ndio maana wamejipanga kuongeza bonasi kutoka sh 150 milioni kwenye ushindi wa nyumbani kwenda milioni 200, kiasi ambacho rasmi wachezaji watatangaziwa leo au kesho kambini. Lakini mmoja wa vigogo wa Simba amedokeza kuwa dakika za mwisho kabla ya wikiendi dau hilo linaweza kupanda zaidi kwani kuna wadau wenye mapenzi na Simba wanajipanga kimyakimya.
Hata hivyo, bonasi hiyo imeongezwa kwa ushindi tu na kama watatoa sare basi watavuta sh 50 milioni iliyozoeleka na wakifungwa basi watatoka patupu.