HARRIS AMSHINIKIZA NETANYAHU KUMALIZA MGOGORO WA GAZA, AKISEMA ‘NI WAKATI MWAFAKA SASA’

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris – ambaye anatarajiwa kuwa mteule wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Novemba – amefanya kile alichokiita “mazungumzo ya wazi na yenye kujenga” na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Akiwa na sauti kali zaidi kuliko Rais Joe Biden, Bi Harris alisema aliweka wazi “wasiwasi wake mkubwa” kuhusu majeruhi huko Gaza, akimweleza Bw Netanyahu jinsi Israeli ilivyo na haki ya kujitetea.

“Ni wakati wa vita hivi kumalizika,” alisema baada ya mazungumzo yao ya ana kwa ana katika Ikulu ya White House.

Bibi Harris pia alisisitiza haja ya njia ya suluhisho la serikali mbili, huku akitoa wito kwa Wamarekani kufahamu “uzito” juu ya mzozo huo.

Mapema siku ya Alhamisi, Bw Netanyahu alikutana na Bw Biden, ambaye alijiuzulu kutoka kwa kampeni yake ya kuchaguliwa tena Jumapili.

Mikutano ya Bw Netanyahu katika Ikulu ya White House ilikuja siku moja baada ya kutoa hotuba kali kwa Congress, akiapa “ushindi kamili” dhidi ya Hamas, huku maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina wakiandamana nje.

Waziri Mkuu anakabiliwa na shinikizo ndani na nje ya nchi ili kumaliza vita vya Israel na Gaza, ambavyo sasa ni mwezi wa tisa.

-BBC