Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia miradi ya maendeleo katika maeneo yao na kuhakikisha inakamilishwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.
“Kwenye usimamizi wa miradi, hakikisheni mnazo taarifa za utekelezaji; hii ni fursa yenu ya kujua miradi yote tangu mwaka 2021, angalieni miradi gani imepata fedha, na mjiridhishe kama imekamilika. Kama haijakamilika, fuatilieni kwa nini,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo leo Jumatatu, Julai 22, 2024, wakati akiongea na Kamati za Usalama za Mikoa na Wilaya pamoja na viongozi wa CCM kwa njia ya video conference kutoka ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni, Dar es Salaam.
Amesema miradi inayojengwa kwa fedha za Serikali kwenye Halmashauri na Manispaa ni mingi, na amesisitiza ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba, 2024 ili ianze kutumika mapema. “Matumizi ya miradi hii ni faraja kwa wananchi na ndiyo matamanio yao,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kupata taarifa za utekelezaji wa miradi na kufuatilia sababu za kutokamilika kwa miradi ambayo bado haijakamilika.
