BEI ZA MAFUTA ZASHUKA MWEZI AGOSTI KUPUNGUZA MZIGO WA GHARAMA KWA WANANCHI.

DAR ES SALAAM , Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo Agosti 5, 2026, imetangaza kupungua kwa bei za nishati ya mafuta nchini kwa bidhaa zinazopitia Bandari ya Dar es Salaam, kutokana na mabadiliko chanya ya bei katika soko la dunia ambapo hatua hiyo imeshuhudia bei za mafuta zikishuka hadi Sh3,898 kwa lita ya petroli na Sh3,978 kwa dizeli ikiwa ni mkakati wa kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa walaji nchini Tanzania, licha ya kuendelea kwa misukosuko ya kiusalama inayovuruga soko la kimataifa nchini Mashariki ya Kati.

Mwenendo huo umeendelea kujidhihirisha baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), leo Agosti 5, 2026, kutangaza bei mpya za mafuta zilizoonyesha punguzo ikilinganishwa na bei za mwezi Julai, na hivyo kuendeleza mwelekeo wa kushuka kwa gharama za mafuta nchini.

Kwa mujibu wa bei hizo mpya, petroli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam sasa itauzwa kwa Shilingi 3,898 kwa lita, kutoka Shilingi 3,990 mwezi Julai. Bei ya dizeli imepungua kutoka Shilingi 4,182 hadi Shilingi 3,978 kwa lita, huku mafuta ya taa yakishuka kutoka Shilingi 4,443 hadi Shilingi 4,003 kwa lita.

Kupungua kwa bei hizo kunatekeleza ahadi iliyotolewa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Nishati Bungeni jijini Dodoma. Alieleza kuwa taasisi zilizo chini ya Wizara, ikiwemo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na EWURA, zitaendelea kuhakikisha wananchi wananufaika na mabadiliko chanya ya bei yanayotokea katika soko la dunia.

“Kadri mafuta yanavyoendelea kuingia nchini kwa gharama nafuu zaidi, ndivyo bei zake zitakavyoendelea kushuka na wananchi wataendelea kunufaika,” alisema Mhe. Ndejembi leo hii jijini Dar es salaam.

Chini ya uongozi wa Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa upatikanaji wa mafuta nchini kupitia Sera na mikakati mbalimbali inayolenga kuhakikisha kunakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta wakati wote, pamoja na kuweka mazingira yanayowezesha wananchi kufaidika na mwenendo mzuri wa bei katika soko la dunia.

hali hiyo ikitarajiwa kuongeza utulivu wa sekta na kupunguza gharama za maisha kwa watanzania.