
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amemtaka Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Naziad Mkeremy, kutumia nafasi yake kuimarisha diplomasia ya uchumi kati ya Tanzania na Malaysia, kwa kuzingatia fursa za uwekezaji, biashara na utalii.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 17, 2026, alipokutana na Balozi Mkeremy katika Ikulu ya Zanzibar, aliyefika kwa ajili ya kuaga kabla ya kuelekea nchini Malaysia kuanza majukumu yake mapya ya kibalozi.
Katika mazungumzo hayo, Rais Mwinyi amesisitiza umuhimu wa balozi kutumia nafasi hiyo kuitangaza Zanzibar kama eneo lenye fursa mbalimbali za uwekezaji, hususan katika sekta za utalii, ujenzi wa hoteli na makaazi, uvuvi, mafuta na gesi, pamoja na maeneo mengine yanayohusiana na Uchumi wa Buluu.
Amesema kuimarishwa kwa diplomasia ya uchumi kunaweza kuchochea mtiririko wa mitaji kutoka Malaysia kwenda Zanzibar, kupanua masoko ya bidhaa na huduma, pamoja na kuongeza fursa za biashara kati ya pande hizo mbili.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amemtaka Balozi Mkeremy kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa Zanzibar na Malaysia katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na kutafuta fursa zaidi za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar na Tanzania, pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya nchi hizo.
Kwa upande wake, Balozi Mkeremy amemshukuru Rais Dkt. Mwinyi kwa maelekezo hayo na kuahidi kuyatekeleza kwa ufanisi katika kituo chake kipya cha kazi nchini Malaysia.
Amesema atatumia nafasi yake kuendeleza maslahi ya Tanzania na Zanzibar nchini Malaysia, kwa kuzingatia maeneo yaliyoainishwa na Rais, ikiwemo uwekezaji, biashara, utalii, elimu na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Malaysia.
Maelekezo hayo yanaelekeza zaidi juhudi za uwakilishi wa Tanzania nje ya nchi katika kutumia diplomasia kama nyenzo ya kukuza uchumi, kuvutia uwekezaji na kufungua masoko mapya kwa fursa zinazopatikana Tanzania na Zanzibar.
