
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeufunga kwa muda Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya kurekebisha eneo la kuchezea kwa kupanda nyasi mpya.
Katika eneo la Uwanja wa New Amaan Complex, kuna viwanja vitatu ambapo viwili hutumika kwa ajili ya mazoezi, na mkubwa unaotumika kwa mechi za mashindano mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Moh’d Makame, wakati akitoa taarifa kuhusiana na maandalizi kuelekea AFCON 2027.
“Uwanja wa New Amaan Complex tumeufunga kwa muda kuimarisha nyasi kwa ajili ya mashindano ya AFCON, tutapanda mbegu mpya na mchakato huo utachukua miezi miwili kupanda, kuota na kuanza kukatwa,” amesema.
Hizi hapa ni sababu tatu kuu zilizolazimisha mamlaka kuchukua maamuzi hayo magumu lakini ya lazima:
Oparesheni ‘Nyasi Mpya’ Kuelekea AFCON: Uwanja huo unaandaliwa rasmi kwa ajili ya kutumika kama uwanja wa mazoezi (Training Ground) kwa timu zitakazoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027). Ili kukidhi viwango vya kimataifa, uwanja unalazimika kuondoa nyasi za zamani na kupanda mbegu mpya kabisa za kisasa.
Mbio Dhidi ya Saa za Ukaguzi wa CAF: Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linatarajiwa kutua visiwani humo kufanya ukaguzi wa mwisho na majaribio ya viwanja ifikapo Januari 2027. Mchakato wa kupanda mbegu, kuota, na kukata nyasi unachukua miezi miwili, hivyo serikali imeamua kuwahi mapema ili kuepuka lawama na uwezekano wa kufungiwa.
Uchovu na Kuchakaa kwa Kapeti la Sasa: Nyasi zinazoondolewa zimekuwa zikitumika mfululizo kwa takribani miaka miwili tangu uwanja huo ulipofunguliwa baada ya ukarabati mkubwa. Kutokana na ratiba ngumu ya mechi za ndani na kimataifa, nyasi hizo zimepoteza ubora unaotakiwa na CAF kwa mashindano makubwa kama AFCON.
