TANZANIA NA DRC KUJIKITA KATIKA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hasan amempokea na kufanya mazungumzo ya ushirikiano na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC ) Mhe.Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo baada ya kuwasili Ikulu ndogo ya Zanzibar, tarehe 18 Agosti, 2026, katika hatua za kuimarisha biashara, usalama, uwekezaji na matumizi ya rasilimali kwa lengo la kukuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi hizo mbili na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,

Mwelekeo huo umetajwa katika mazungumzo kati ya viongozi wa Tanzania na DRC, ambapo wameangazia umuhimu wa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika biashara, kuboresha huduma za mipakani na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika utekelezaji wa fursa za kiuchumi.

Katika eneo la miundombinu, viongozi hao wamezungumzia umuhimu wa kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa miradi ya kimkakati, ikiwemo reli, barabara na huduma za bandari. Ushirikiano huo unalenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa miundombinu na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika ukanda.

Tanzania pia imeeleza fursa zilizopo katika sekta za kilimo, uvuvi na mifugo, huku DRC ikialikwa kushirikiana katika biashara na uwekezaji kwenye maeneo hayo. Hatua hiyo inalenga kuongeza fursa za masoko na kuimarisha biashara baina ya nchi hizo mbili.

Sekta ya madini ni miongoni mwa maeneo yaliyopewa umuhimu katika ushirikiano huo. Tanzania na DRC zina rasilimali nyingi za madini na zimeeleza dhamira ya kubadilishana uzoefu na ujuzi katika uchimbaji, uongezaji thamani, utafiti pamoja na upatikanaji wa masoko ya madini.

Katika kuendeleza ushirikiano huo, DRC imealikwa kutumia fursa zinazopatikana katika kituo cha madini kilichopo Tanzania kwa ajili ya kubadilishana maarifa, ujuzi na kufanya tafiti zinazohusiana na sekta ya madini.

Mbali na masuala ya uchumi, mazungumzo hayo yamejumuisha amani na usalama kama nguzo muhimu katika maendeleo ya ukanda. Tanzania imeeleza kuunga mkono juhudi za kutafuta amani na utulivu wa kudumu nchini DRC na kutatua changamoto za kiusalama zinazoathiri maendeleo.

Aidha, viongozi hao wamegusia usalama wa afya na hatua za kukabiliana na magonjwa ya milipuko, ikiwemo Ebola. Ushirikiano katika eneo hilo unalenga kuimarisha hatua za kinga na udhibiti wa magonjwa ili kulinda afya na usalama wa wananchi.

Kwa mtazamo mpana, mwelekeo wa Tanzania na DRC unaonesha jitihada za kujenga ushirikiano wa kimkakati unaohusisha uchumi, miundombinu, biashara, uwekezaji, madini, uzalishaji, afya na usalama. Ushirikiano huo unatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kukuza maendeleo ya nchi hizo mbili na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika Afrika Mashariki na Kati.